Je kunena kwa lugha hutoka kwa Mungu ama Kwa shetanI?
Kitu
cha muhimu cha kufahamu kuhusu kunena kwa lugha ni alichokisema Yesu kuhusu
kunena kwa Lugha. Marko 16:17
“Na ishara
hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha
mpya;…..”
Bwana
Yesu, alishuhudia kuwa kunena kwa lugha ni alama ya nguvu ya Mungu kwa hao
waaminio. Mungu hakuwapa Watoto wake karama zilizo mbaya; kwa mantiki hiyo
hatuogopi ama kuikashifu karama yeyote ya Roho Mtakatifu ikiwemo kunena kwa
Lugha.
Watu
wengine wanasema, wakristo walio wengi hunena kwa kuigiza kwa watu wengine.
Hilo linabaki kuwa siri ya anenaye na Mungu wake. Ila anenaye na kwa Lugha
anazo faida nyingi. Inamsaidia
kuwasiliana moja kwa moja na Mungu.
Kulingana
na mtume Paulo, katika 1 kor 13:1 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za
malaika, kama sina upendo , nimekuwa kama shaba iliayo na upatu uvumao.”
Unapopokea
karama ya kunena kwa lugha Roho Mtakatifu anadownload lugha na kuhifadhi kwenye
roho yako bila wewe kuisoma hiyo lugha. Niseme wazi kuwa ni Lugha na sio kaneno
kanakojirudia rudia manake huwezi kuomba ama kuongea na Mungu kwa neon moja.
Mwaka
2006, Dr. Andrew Newberg wa chuo kikuu cha Pennsylvania alichukua picha za
ubongo za watu watano waliokuwa wakinena kwa lugha, baada ya utafiti wake
alisema, “ tumeona mabadiliko makubwa kwenye uwezo wa kufanya kazi wa ubongo na
kugundua kutokuwepo uwezo wa binafsi wa ubongo wa kufanya kazi, hii inaonyesha
uwezo wa ziada wa kuzungumza bila mzungumzaji kujitambua…hili ni jambo la ajabu”
alisema. Hii ina maana kuwa kunena kwa lugha ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
1.
Je kunena kwa lugha ni zawadi maalumu
kwa watu maalumu?
Kunena kwa
lugha imeonekana sana kama karama ya Roho mtakatifu katika agano Jipya. Katika
Mdo 2:4, biblia inasema kuwa wanafunzi wa mwanzo 120 walinena kwa Lugha katika
chumba cha juu; “wote walijazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa Lugha nyingine,
kama Roho alivyowajalia kutamka”
Hatujui kama
wote walipokea kipawa cha Imani ama kuponya ama kutoa pepo, lakini tunajua kwa hakika
kuwa walinena kwa lugha mpya kama Roho alivyowajalia.
Leo kuna
wakristo waongofu wengi sana duniani, na wanaomwamwini Kristo, na wanatengeneza
kundi kubwa linalokuwa kwa haraka sana duniani. Karama ya kunena kwa LUGHA sio
ya kundi dogo lililochaguliwa na Roho Mtakatifu bali ni kwa wote wanaomwamini
Bwana Yesu na wanao amini kazi za Roho Mtakatifu. Mtume Paulo amelisema wazi
katika 1Kor 14:5 kuwa “Nami nataka ninyi nyote mnene kwa Lugha,
lakini Zaidi sana mpate kuhutubu, maana yeye ahutubuye ni mkuu kuliko yeye
anenaye kwa lugha, isipokuwa afasiri, ili kusudi kanisa lipate kujengwa”
Kwa mantiki
hii Matume Paulo anatamani kila mtu anene kwa lugha kwa ajili ya kujijenga
kiroho Zaidi na kuhutubu kwa ajili ya kulijenga kanisa.
2. Je karama
hii iliisha baada ya karne ya kwanza ama hadi sasa inafanya kazi?
Kuna baadhi
ya wasomi wa Dini wanao amini kuwa karama za Roho Mtakatifu ziliishia karne ya
kwanza (the doctrine of cessationism). Kwenye andiko hili wanaamini kuwa karama
zote za roho mtakatifu ziliisha baada ya wanafunzi 12 kufariki. Lakini kuna
maandiko ya mababa wa Imani kama Justin Martyr (100-165), Irenaeus (115-202),
Turtullian (160 -220) na Origen (185 -254) wanashuhudia kuwepo kwa karama hizi ikiwemo
kunena kwa Lugha wakati wakihudumu katika kanisa enzi zao muda mrefu baada ya Mtume
Yohana kufariki miaka 100 baada ya Kristo.
Mtume Petro
anashuhudia katika Mdo 2:39 kuwa karama ya kunena kwa lugha ni kwa wote
walioitwa na Mungu; “kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa wote
walio mbali na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”
Mtume Paulo pia
anaandika katika 1kor 13:8,9 kuwa ile iliyokamili itakapokuaja, kunena kwa
lugha kutakoma. Hii ni ina maana atakapokuja Kristo (iliyo kamili) kwa mara ya
pili ndipo karama hii na nyinginezo zitakoma. Maana biblia inafundisha kuwa hakuna
aliye mkamilifu ila mmoja ndiye Yesu. Atakapokuja hatutakuwa na haja ya kunena
kwa lugha kuwasiliana na Mungu kwa maana tutakuwa naye. Kwa mantiki hii karama
ya kunena kwa lugha ipo kwa kila mwamini anayetaka kuipokea.
3. Watu husema
nini wanaponena kwa Lugha?
Biblia inafundisha
mambo matano makuu matano mtu anapoomba kwa lugha:
a)
Anawasiliana moja kwa moja na Mungu.
1Kor14:2 “maana
yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna
askikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.”
Kunena kwa
lugha ni njia ya moja kwa moja ya kuwasiliana na Mungu.
b)
Wanasifu matendo makuu ya Mungu
Katika Mdo
2:11, “……; tumewasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu”
Mbali na kuwa
ni ujinga (kama wengine wasemavyo) kunena kwa lugha kunamtukuza Mungu na
matendo yake makuu kwetu. Hii inawezaje kuwa jambo baya?
c)
Wanamwadhimisha Mungu.
Katika Mdo
10:46, “kwa maana waliwaskika wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu….”
Hata kama
hatuelewi tunachosema tunaposema kwa Lugha tunajua kuwa tunamwadhimisha Mungu
katika Roho (1kor 14:16)
d)
Wana jijenga wenyewe kiroho
Mtume Paulo
anasema katika 1Kor 14:4, “Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye
hulijenga kanisa.”
Kunena kwa
lugha ni kama karakana ya kiroho, unajijenga kiroho na kuwa imara pia kiroho.
e)
Roho Mtakatifu anasali ndani yao.
Katika kitabu
cha Warumi 8:26,27, “ …….kw maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho
mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa……kwa kuwa huwaombea
watakatifu kama apendavyo Mungu.
Kuomba kwa
Roho huleta ufunuo na maono ya mapenzi ya Mungu kwako. Hivyo kunena kwa Lugha
ni kiungo muhimu cha kuombewa na Roho mtakatifu.
Kama
hauna Imani juu ya karama ya kunena kwa lugha ama ulishakuwa na mtazamo hasi
kuhusu karama hizi nakutia moyo kusoma biblia na kuomba ufunuo wa kimaandiko
kuelewa. Mwombe Roho Mtakatifu akufunulie ukweli kuhusu karama hii.
Wako
pia watu wengi waongofu, wanaotamani kunena kwa lugha, kwa bahati mbaya badala
ya kutulia na kumwomba Mungu wanaiga unenaji wa watu wengine ili tu waonekane
nao wananena kwa lugha. Hii sio nia ya Roho mtakatifu na ni dhambi kudanganya
nafsi yako na wanaokuzunguka.
Kama
nlivyotangulia kusema, lugha inakua vivyo hivyo na lugha ya Roho Mtakatifu,
unaponena mara kwa mara Mungu anakuongezea misamiati na unakuwa na upeo mpana
wa kuongea Lugha ya Roho Mtakatifu.
Yesu
anasema katika Luka 11:13, “ basi ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto
wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu
hao wamwombao”?
Wakati
mwingine twatakiwa kuomba na kuzidi kuomba mpaka tutakapo pokea tukiombacho. Kama
umevuviwa tayari karama yoyote itumie kila wakati ili izidi kufanya kazi ndani
yako. 1Kor14:18, Paulo anajisifu kuwa; “Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa
lugha Zaidi ya ninyi nyote”
Je
kuna matumizi yasiyo sahihi ya karama ya kunena kwa lugha?
Ndiyo,
bila shaka kuna watu hunena kwa lugha bila utaratibu na kwa matumizi ya tamaa
zao wenyewe na wanahitaji kuelekezwa na kufundishwa. Lakini usimtupe jongoo na
mti wake kwa kukataa kuwepo kwa karama ya kunena kwa lugha kwa ajili ya
matumizi mabaya ya hii karama. Tujifunze kwa mtume Paulo anaposema katika 1Kor
14:39, “kwa ajili ya hayo, ndugu, takeni sana kuhutubu, wala msizuie kunena kwa
lugha.
No comments:
Post a Comment